Usajili unaolenga ni hatua ya usajili inayojaribu kufikia kundi lisilotambulika la wapigakura, mara nyingi kwa sababu kundi hilo lina viwango vya chini vya usajili kuliko watu wote kwa jumla. Miongoni mwa makundi haya ambayo yanaweza kulengwa ni wapigakura vijana, watu kutoka makabila fulani, maskini na wasio na makazi, wanawake, wapigakura wanaoishi ughaibuni, na wapigakura wanaohamahama mijini.
Wapigakura vijana
Kwa kuwa viwango vya upigaji kura kihistoria vimekuwa chini miongoni mwa vijana, halmashauri ya kusimamia uchaguzi inaweza kuweka mkakati wa kuzidisha usajili wa wapigakura vijana. Kama sehemu ya hatua hiyo, inaweza kubuni mpango wa elimu kwa wapigakura unaowalenga vijana; huu unaweza kutumiwa pia kama kipengele cha mipango ya elimu kwa raia inayotekelezwa katika shule za upili. Ili kuwasisimua vijana na kuwashirikisha katika mchakato wa upigaji kura, halmashauri ya kusimamia uchaguzi inaweza kupanga shughuli za umma, kwa matukio kama vile “Tingisha Kura” yaliyofanywa hivi majuzi katika nchi nyingine. Halmashauri ya kusimamia uchaguzi inaweza pia kutengeneza orodha rejista ya muda ya vijana watakaofikisha umri wa kupiga kura katika mwaka mmoja au miwili hivi baadaye; punde wanapofikisha, wanaweza kuhamishiwa moja kwa moja kwenye orodha ya jumla ya wapigakura.
Watu kutoka Jumuia za makabila fulani
Watu kutoka makabila fulani wanaweza kukabiliwa na matatizo makubwa ya lugha katika kushiriki katika uchaguzi. Wanaweza pia kuwa na uelewa mdogo au wasielewe kabisa mchakato wa kidemokrasia au haki yao ya kujisajili na kupiga kura. Ili kukabiliana na watatizo kama hayo, halmashauri ya kusimamia uchaguzi inaweza kuweka taarifa kuhusu uchaguzi katika lugha nyingi. Mazungumzo na viongozi wa kabila fulani yanaweza kusaidia kutambua mikakati ya kuhusisha kikamilifu jumuia hiyo katika mchakato wa uchaguzi.
Maskini na Wasio na makao
Watu maskini kabisa katika jamii wana uwezeekano mdogo wa kujisajili au kushiriki katika maisha ya kisiasa. Wakati mwingine kanuni za usajili huwahitaji wapigakura kuwa na makao maalumu; wale wasioafiki hitaji hilo wanaweza kuzuiwa kabisa dhidi ya kujisajili. Suluhisho linaweza kuwa kuruhusu watu hawa kutumia makazi yasiyo na wenyewe katika jumuia zao. Katika mji ulio na zaidi ya eneo pana moja la uchaguzi, watu wasio na makazi wanaweza kupewa makazi katika maeneo maalumu katika kipindi kizima cha uchaguzi; matokeo yatakuwa kwamba wamesajiliwa katika takribani idadi sawa katika kila eneo la uchaguzi, hivyo basi kusawazisha athari ya kusajili kundi hili la wapigakura.
Wanawake
Jamii nyingine bado zinashikilia vizingiti vya kijamii na kitamaduni, iwapo si vya kisheria, dhidi ya kushiriki kwa wanawake katika siasa. Kampeni ya usajili inayolenga wanawake inaweza kujaribu kuwapa uwezo wa kufikia nyenzo za elimu kwa wapigakura hivyo basi kuwahimiza kujisajili na kupiga kura; nyenzo hizo huwekwa katika maeneo ambako wanawake wana uwezo wa kuziona. Halmashauri nyingi za kusimamia uchaguzi hushirikiana na mashirika ya wanawake ili kueneza ujumbe huo vilivyo.
Wapigakura wanaoishi ughaibuni
Idadi inaendelea kuongezeka ya watu wanaosafiri kutoka kwao hadi maeneo ya mbali wakitafuta kazi, na wengi wakienda katika nchi za ughaibuni. Wengine huacha wachumba na watoto wao huku wakifanya kazi ughaibuni kwa muda mrefu. Licha ya kutokuwepo kwao, wao huendelea kudumisha uhusiano wa karibu na nchi yao kiasili na kujitambulisha nayo. Juhudi za usajili unaolenga watu kama hao zinweza kujumuisha hatua maalumu za halmashauri ya kusimamia uchaguzi kuyatembelea maeneo hayo ya kigeni ili kuwasajili wapigakura, au kwa shughuli ya elimu kwa wapigakura na kuwashauri kuhusu haki yao ya kujisajili na kupiga kura na vilevile jinsi ya kufanya hivyo.
Wapigakura wa kuhamahama mijini
Katika maeneo mengi ya miji kwenye demokrasia zilizostawika kiuchumi, takribani asilimia 20 ya watu hubadilisha makazi kila mwaka. Katika nchi inayotumia orodha endelevu, halmashauri ya kusimamia uchaguzi inapaswa kufanya juhudi za kutosha kufuatilia mabadiliko kama hayo katikati ya chaguzi. Kadiri uchaguzi unavyokaribia, wapigakura wengi kama hao (ambao huenda wengi wakawa vijana) wanaweza kusajiliwa visivyo. Shughuli ya usajili unaolenga kundi kama hili inaweza kuhusisha kampeni ya elimu kwa wapigakura pamoja na hesabu ya usajili inayolenga nyumba hadi nyingine.