Sajili ya raia ni orodha ya taarifa za kimsingi kuhusu raia wote (k.m. jina, jinsia, uraia, umri, hali ya kindoa na anwani). Huhifadhiwa na serikali. Kujumuishwa kwenye orodha hiyo ni kwa lazima na raia huhitajika kuripoti badiliko lolote kwenye taarifa yake kwa maofisa wanaotunza orodha hiyo (hasa wizara ya mambo ya ndani). Kwa kawaida, serikali zinazotunza sajili ya raia huitumia kutengeneza orodha ya wapigakura. Matokeo ni kwamba kwa kila raia anayeafiki mahitaji ya kupiga kura, kujumuishwa kwenye sajili ya raia humaanisha kuwekwa pia kwenye rejista ya wapigakura.
Sajili ya raia hutgemea kwa kiwango kikubwa kitambulisho cha taifa kwa kila raia, bali orodha endelevu haitegemei. Masuala ya kitamaduni huonekana kuwa na mchango mkubwa katika maamuuzi kuhusu ikiwa ni bora kutumia nambari ya kitambulisho cha kitaifa kwa raia. Katika jamii ambazo zimeamua kutumia kitambulisho hicho cha kitaifa matumizi ya kitambulisho hiki huwezesha taarifa kuwahusu raia kutunzwa vizuri tena upana. Yamkini matumizi ya nambari hiyo yanaambatana na utunzaji wa orodha ya raia. Jamii nyingine huonekana kupinga matumizi ya kitambulisho cha kitaifa na mara nyingi huweka mipaka katika kuonyeshana nambari zao za vitambulisho kama nambari za siri au za bima ya jamii miongoni mwa mashirika mengine. Jamii ambazo hukataa matumizi ya nambari za vitambulisho vya kitaifa kwa raia pia mara nyingi huchagua kutobuni sajili za raia.
Tajriba ya Wadeni
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Udeni hueleza tajriba ya Wadeni ya kuunganisha sajili ya kitaifa ya raia na orodha ya wapigakura:
Ni jambo la lazima katika uchaguzi kwa mpigakura mtarajiwa asajiliwe katika rejista ya uchaguzi (orodha ya wapigakura). Sajili ya kitarakilishi ya uchaguzi hutegemea taarifa zilizopo kwemye mfumo wa kitaifa wa kusajili raia (ambao pia husimamiwa na Wizara ya Mambo ya Ndani) ambamo halmashauri kuu huwasilisha taarifa ya kimsingi na inayohusiana na usimamizi kuhusu raia ikiwemo kupata haki za kupiga kura, mabadiliko kwenye anwani na vifo. Kwa hivyo, kujumuishwa kwa haya kwenye rejista ya uchaguzi – na mabadiliko kutokana na mabadiliko ya makao nk – hufanyika moja kwa moja na bila kukoma. Kwa sababu hii, sajili hiyo husasaishwa vya kudumu na ni watu wanaoishi ughaibuni pekee … wanaopaswa kuchukua hatua hiyo. Wanapaswa kutuma maombi ya kujumuishwa kwenye orodha ya baraza ambako walikuwa na makao ya kudumu kabla ya kuhamia ughaibuni.
Chapisho hutolewa la rejista iliyosahihishwa vya kudumu nay a kitarakilishi kukiwa na siku 18 kabla ya uchaguzi kama siku ya marejeo. Wapigakura watarajiwa wanaoingia nchini humo baada ya tarehe hii hawawezi kujumuishwa katika rejista hiyo kabla ya uchaguzi na hivyo basi hawaruhusiwi kupiga kura. Watu wanaohamia katika mabaraza mengine chini ya siku 18 kabla ya uchaguzi mkuu husalia kwenye rejista ya wapigakura ya eneo la kwanza hadi baada ya siku ya uchaguzi. mabadiliko katika rejista ya wapigakura kwa sababu ya (1) kuhama, (2) vifo, (3) suala la kuamuliwa kutostahi (kuondolewa) kisheria, na (4) watu kupoteza au kupata uraia wa Kideni ambazo huripotiwa kwa mamlaka za mitaani chini ya siku 18 kabla ya uchaguzi, huingizwa kwa mikono katika chapisho la rejista ya wapigakura. [1]
Matumizi ya sajili ya raia nchini Udeni huhitaji juhudi kubwa. Maafisa wanapaswa kutunza deta inayohitajika kwa uchaguzi pamoja na deta muhimu za kitakwimu ambazo kwa kawaida huhifadhiwa katika sajili ya raia.
Bila shaka, raia wote huhitajika kuarifu mamlaka zinazoshughulika na sajili ya raia kuhusu mabadiliko katika taarifa za kimsingi kuwahusu kwa wakati maalumu – pengine siku 30 kutoka siku ya mabadiliko hayo. Kusasaishwa kwa taarifa kwenye sajili ya raia huchelewa kidogo jinsi inavyokuwa katika rejista endelevu. Kisha, masahihisho yayo hayo hufanywa pia kwenye orodha nyingine kutokana na sajili ya raia, ikiwemo orodha ya wapigakura.
Sajili ya Raia na Usajili wa Wapigakura
Katika nchi au maeneo mengine yaliyo na sajili ya raia kama vile Uswidi, raia hawahitajiki kufanya chochote ndipo wasajiliwe kupiga kura. Ofisi ya kushughulikia ushuru katika mtaa huo hutunza faili zenye usasa kuhusu ustahifu wa kupiga kura na hivyo yeyote aliye kwenye sajili ya raia anasajiliwa moja kwa moja kupiga kura. Katika nchi nyingine kama vile Senegali, raia wanapaswa kutuma maombi ya kusajiliwa kama wapigakura ingawa serikali hutunza sajili ya raia.
Pale ambapo orodha nyingine ya wapigakura inatengenezwa kutokana na sajili ya raia, shughuli hiyo hufanywa karibu kabisa na uchaguzi. kwa kuwa sajili ya raia hutoa taarifa kama siku ya kuzaliwa, jinsia au jina, taarifa haihitaji kukusanywa tena ili kutumiwa katika orodha ya wapigakura. Hili hupunguza wakati unaohitajika kujaza deta na kutayarisha orodha.
Ujenzi na utunzaji wa sajili ya raia ni jukumu kubwa la kiusimamizi hivyo basi huenda likawa ghali. Ubora wa mfumo huo ni kwamba deta nzuri ikishapatikana ya watu wote, taarifa hiyo inaweza kutumika kwa kazi nyingi bila gharama ya ziada kwa mashirika mengine. Kwa mfano, kutumia sajili ya raia kujenga orodha ya wapigakura huhusisha kuongeza kigezo cha ustahifu wa kupigakura kwenye sajili hiyo na kisha kuchukua deta hiyo na kuiwasilisha kwa halmashauri ya kusimamia uchaguzi. Wajibu wa shirika hili katika mchakato huo hufungiwa katika kukagua deta ya deta ya usajili ili kutambua kasoro na kuachwa kwa sehemu nyingine, na kusahihisha kisha kutoa orodha ya mwisho ya kutumiwa siku ya uchaguzi. Kukiwa na sajili ya raia yenye usasa, orodha ya wapigakura inaweza kuundwa kwa gharama ndogo.
MAELEZO
[1] Folketing (Bunge la Kideni),“Uchaguzi wa Ubunge na Usimamizi wa Uchaguzi huko Udeni.