Usajili wa hiari
Usajili wa hiari hutokana na kanuni kwamba upigaji kura ni haki raia na kwamba wapigakura wanaweza kuchagua kujisajili au wakatae.
Bila shaka baadhi ya wapigakura watachagua kutojisajili hivyo basi kujinyima haki yao ya kupiga kura. Ikiwa uwezekano wa kujisajili kupiga kura ni wa kubahatisha au hauna mpangilio maalumu – yaani, ikiwa makundi yote ya raia yanajisajili kwa viwango sawa, wawe wanawake au weanaume, vijana au wazee, wakazi wa mijini au mashambani, matajiri au maskini, walio na viwango vya juu vya masomo au wale wa viwango vya chini, na kadhalika – mwisho unaweza kuwa kwamba usajili wa kujitolea hauna athari kubwa kwa matokeo ya uchaguzi au kwenye uteuzi wa wawakilishi na serikali.
Katika demokrasia nyingi hata hivyo, tofauti zinaweza kuonekana katika ni nani anayeamua kujisajili na yule asiyejisajili. Kwa mfano, pana uwezekano wa wanaume kuamua kushiriki kushinda wanawake, ingawa pengo hilo limekuwa likipungua katika nchi nyingi katika kizazi kilichopita. Pana uwezekano wa vijana wachache tu kujisajili na kupiga kura kushinda raia wa umri wa makamo au wazee. Wapigakura wa mijini hujisajili kwa idadi kubwa kushinda wale wa mashambani, matajiri wanaweza kujisajili kwa viwango vikubwa kushinda maskini, na wale walio na viwango vya juu vya masomo kujisajili kushinda wale walio na viwango vya chini.
Ikiwa wale wanaoshiriki kwa viwango vikubwa wana desturi, hisia na mapendeleo ya kisiasa vinavyotofautiana na vya wale wanaoshiriki kwa viwango vidogo, tokeo huwa kwamba kushiriki huko na usajili wa kujitolea wa wapigakura vitakuwa na atahri kubwa kwenye matokeo ya uchaguzi kwa kupendelea wale ambao idadi kubwa ya wafuasi wao ndiyo huenda ikawa imejisajili na kushiriki. Ikiwa watu wanaojisajili kupiga kura inaegemea upande mmoja au haiwakilishi idadi kubwa ya watu, matokeo ya uchaguzi huo yanaweza kukosa uhalali.
Usajili wa lazima na wa Ulazima-Kiasi
Usajili wa lazima au wenye ulazima kiasi hutokana na kanuni kwamba upigaji kura katika demokrasia si haki ya mtu bali jukumu la uraia. Kuchagua kutojisajili na hivyo kutopiga kura huchukuliwa kama kutotimiza wajibu huo.
Ikiwa upigaji kura ni wa lazima, kama ilivyo nchini Australia, basi usajili pia utakuwa wa lazima hata ingawa huenda ikakosa kutekelezwa kisheria. Katika nchi ambako upigaji kura ni wa lazima mara kwa mara huwa na viwango vikubwa vya kujitokeza kwa wapiga kura kuliko kule ambako upigaji kura ni wa hiari ya mtu binafsi. Isitoshe, ikiwa upigaji kura ni wa lazima, halmashauri ya kusimamia uchaguzi itakuwa na jukumu kubwa la kuwarahisishia watu kujisajili na kupiga kura.
Kule ambako serikali inachukua jukumu la kuanzisha mchakato wa usajili wa wapigakura – k.m. kwa kusajili kutoka nyumba hadi nyingine au kudumisha sajili ya lazima ya raia – usajili huwa karibu na kuwa lazima. Kwa mfano, raia anaweza kukataa kujibu maswajili ya wasajili, japo ombi rasmi la msajili la kutaka kupewa habari huwa pamoja na shinikizo au kuchochea watu kujitolea kujibu na kujisajili. Katika nchi zinazotumia sajili ya raia, mara nyingi raia huwa na wajibu rasmi kisheria kutoa taarifa kuhusu mabadiliko kwenye hali zao binafsi kwa halmashauri ya kusimamia raia. Kwa hivyo, orodha ya wapigakura kutokana na deta kutoka kwa sajili ya raia inaweza kuchukuliwa kama iliyotolewa kwa njia ya usajili wa lazima moja kwa moja.
Usajili wa lazima hutoa orodha pana ya wapigakura wote stahifu na kutoa nafasi ya tathmini linganifu ya kujitokeza kwa wapigakura kama sehemu ya wapigakura wastahifu. Kipimo halisi cha kujitokeza kwa wapigakura katika uchaguzi wowote ni idadi ya watu waliopiga kura ikilinganishwa na idadi ya watu waliofikisha umri wa kupiga kura, na kiwango hiki kinaweza kudhihirisha ufaafu wa mpnago wa usajili wa wapigakura.
Katika mfumo usajili wa lazima, raia huelewa kwa ukamilifu kwamba upigaji kura ni wajibu na jukumu la raia. Maana halisi ya mfumo wa usajili na upigaji kura wa lazima ni kwamba kila raia ana wajibu wa kupiga kura kwa niaba ya nafsi yake na kwa niaba ya jumuia yake pana. Yaani, raia wana wajibu kupiga kura kwa manufaa ya mfumo wa demokrasia, sio tu kwa nia ya kutaka hisia zao ziwakilishwe.