Demokrasia ni dhana inayovutia, na ongezeko la idadi ya mataifa yanayofuata maadili ya kidemokrasia yameashiria maisha tofauti kwa watu wengi ambao sasa wanaishi katika uhuru kutoka kwa utesi wa kisiasa au uongozi wa kiimla. Kwa wengi, hasa wale katika demokrasia mpya, ni dhana pana na kuelewa maana yake katika utendaji huchukua muda mrefu. Kuna maelezo mengi kuhusu demokrasia, na wajibu wa watoaji elimu ni kuweka wazi maelezo haya kwa wasomi katika kiwango kifaacho. Kwa kuwa demokrasia ni dhana inayohusisha sehemu za tabia, ujuzi, maarifa na mitazamo na vilevile masuala ya kisiasa na uongozi, inatoa changamoto spesheli.
Namna ambavyo wanaotoa elimu wanavyofanya kazi na kufunza vitaathiri uelewa ambao watu wako nao kuhusiana na dhana ya demokrasia. Kutokana na hayo kuna mjadala katika maandishi yanayo husu methodolojia au mbinu za elimu ya kidemokrasia- kuthamini muingiliano, ushirika na mchango wa kibinafsi, kwa mjadala na ugunduzi wa maana.
Kuna habari fulani za kimsingi ambazo zinatoa msingi bora wa kukuza uelewaji na uthamini wa demokrasia.
Kueleza Demokrasia
Kwa sababu dhana ya demokrasia ni changamano na yenye kushindaniwa, kila mara kutakuwa na tofauti za kimaoni, ingawa kuna makubaliano kwa kiasi fulani kuhusu maelezo ya kimsingi dhana hii. Nyingi ya fafanuzi za demokrasia inalenga sifa, taratibu, na taasisi. Kwa kweli kuna madhihiriko mingi ya demokrasia katika ulimwengu halisi na wanaoelimisha Wapigakura hawataki kuchukulia kuwa taratibu na tamaduni fulani mahususi zinafaa kuchukuliwa na kukuzwa katika ulimwengu wote. Uelewa wa kibinafsi wa anayeelimishwa, tajriba na imani, na historia ambayo nchi yake mahususi imepitia, inafaa kuletwa pamoja ili kuunda ufafanuzi ambao unaleta maana na ambao unawezekana katika maisha yao ya kila siku.
Demokrasia haihusishi seti moja ya kipekee ya taasisi ambayo inatumika ulimwenguni kote. Umbo mahususi ambalo demokrasia huchukua katikanchilinategemea pakubwa na hali ya kisiasa, kijamii, na kiuchumi na kwa kiwango kikubwa inaathiriwa na historia, itikadi, na tamaduni za nchi hiyo.
Maandishi mengi kuhusu demokrasia huanza kwa kutambua ni wapi neno hilo lilitoka na ni wapi uzingatiaji wa taratibu za kidemokrasia ulikonakiliwa na kurasimishwa kwanza. Maandishi hayo pia hutoa fafanuzi za demokrasia ambazo zimetumika kwa muda mrefu. Zifuatazo ni baadhi ya fafanuzi, kuanzia kwa ile ambayo ni sahili hadi kwa ile changamano. Fafanuzi hizi zinaweza kutumika kuleta uelewa katika fafanuzi ambazo wasomi wenyewe wamezibuni katika mijadala.
“Demokrasia
inatokana na neno Kigiriki demos
lenye maana ya ‘watu’ na kratos lenye
maana mamlaka au uwezo.” [1]
“…
serikali ambayo inaendeshwa kutokana na
kibali kilicholewa kwa hiari.”[2]
“…
mfumo wa serikali ambao mamlaka kuu yamo mikononi mwa watu.”[3]
“Uongozi
wa watu katika nchi moja kwa moja au kupitia kwa uwakilishi.”[4]
“Mfumo
wa serikali ambamo uongozi wa kisiasa unatekelezwa na watu, aina moja kwa moja
au kupitia kwa waakilishi wao waliochaguliwa.”[5]
“Neno
demokrasia lenyewe linamaanisha uongozi wa watu. Demokrasia ni mfumo ambao watu
wanaweza kubadilisha viongozi wao kwa njia ya amani na serikali inapewa haki ya
kuongoza kwa sababu watu wanasema kuwa inaweza.”[6]
Mianzo ya Demokrasia
Neno demokrasia liliundwa na Wagiriki wa kale ambao wakianzisha mfumo wa moja kwa moja wa serikali mjini Atheni. Wanaume wote wazima wangekusanyika kujadili maswala na wange piga kura kwa ishara ya mikono. Watumwa na wanawake hawakuwa na haki ya kupiga kura. Serikali ya aina hii inachukuwa muda mwingi na haiwezekani kwa watu wengi kukutana kila wakati ambapo uamuzi unapaswa kutolewa.
Kwa hivyo, hatua kutoka kwa demokrasia ya moja kwa moja (ambayo watu wanapiga kura moja kwa moja kwa maswala) hadi kwa demokrasia ya uwakilishi (ambayo watu wanapigia kura wawakilishi au wanasiasa ambao wanafanya uamuzi kwa niaba yao) haingeweza kuepukwa hatua kwa sababu jamii kubwa na pana zilianzisha demokrasia.
[7]
Leo hii kuna aina za demokrasia kama vile kura za maamuzi, malalamishi, maoni, na mapendekezo, lakini haya hutokea mara nyingi katika demokrasia kongwe zaidi na zilizoendelea kiteknolojia.
Demokrasia hivi sasa
Demokrasia ipo ili kutoa njia kwa watu kuishi na kuwa pamoja kwa njia ambayo ni ya manufaa kwa wote. Ingawa nyingi katika demokrasia za sasa haziwezi kuwa zilikuwepo kabla ya vita vya pili vya dunia, kuna mifano ya aina za serikali katika jamii nyingi za kale ambako maadili ambayo watu wengi waliamini kuwa yanaongoza viongozi na jamii katika njia ambazo uamuzi na kanuni ziliundwa, na katika njia ambapo wanajamii walitendewa na kuishi pamoja.
Imedaiwa kuwa demokrasia ni dhana geni katika bara la Afrika, dai ambalo linatokana na mkanganyiko baina ya maadili ya kidemokrasia na midhihiriko yake kitaasisi. Kanuni za kidemokrasia zinaushisha ushiriki mpana, idhini ya watawaliwa na uajibikaji kwa umma wa wale walio mamlakani- kanuni ambazo zilidhihirika katika mifumo ya kisiasa ya jamii ya Kiafrika ya kale.[8]
Mpito ya kisiasa hadi kwa taifa la kidemokrasia na vile vile ukarabati unaohitajika kama vile upigaji kura na uchaguzi, katiba, na au mahakama huru inaweza kuwa mzito kwa wananchi wapya. Kwa sababu hii kulenga kwenye tajriba za kibinafsi za watu kutakuwa njia muhimu ya kuwafanya watu kuwa na uelewa sawa na wa kiutendaji kuhusu demokrasia.
Waelimishaji wanaowafunza wananchi kuhusu demokrasia wanafaa kuhimiza watu kutoa maoni yao kuhusu maadili ambayo tayari yapo katika namna watu wanavyoingiliana na wengine katika jamii katika maisha ya kila siku. Kutokana na mkusanyiko huu wa maadili mwelimishaji ataweza kujitokeza na kundi la matamanio na maadili yanayoimarisha demokrasia ambayo ni matakwa ya mteja. Hii itaweka misingi muhimu ambayo itaweza kutalii mfumo wa uongozi ambao unapatikana katika nchi yao na kiwango ambacho inaweza kuelezwa kama ya kidemokrasia.
Demokrasia ya uwakilishi
Kila mtu ana haki ya kushiriki katika serikali ya nchi yake, moja kwa moja au kupitia wawakilishi waliochaguliwa kwa hiari. Nia ya watu itakuwa katika msingi wa mamlaka ya serikali; hii itadhihirishwa katika chaguzi za mara kwa mara za kweli ambazo zitaruhusu usawa na upigaji kura na watu wote na zitafanyika kwa njia ya siri au taratibu nyingine huru za kupiga kura ambazo ni sawa hivyo.[9]
Upigaji kura ni mojawapo ya mikakati ambayo uongoza nchi ya kidemokrasia na huwafanya viongozi kuajibika, na pia ni kigezo cha kuwawezesha viongozi kujua jinsi ambavyo wametenda katika uongozi. Wakati wa uchaguzi wananchi humpigia kura mgombezi wampendaye. Wagombezi ambao wamechaguliwa au wawakilishi huwa serikali ya nchi. Viongozi waliochaguliwa huwakilisha watu na utawala kwa kipindi fulani ofisini. Wawakilishi huchaguliwa kupitia chaguzi chini ya misingi ya jimbo la uchaguzi au mfumo sawa wa uwakilishi, au mchanganyiko wa yote mbili.
Waelimishaji wa raia katika nchi wataamua kusisitiza na kueleza kwa undani aina ya demokrasia ya uwakilishi ambayo imechaguliwa. Zaidi ya hayo, kuieleza na pia kueleza tofauti zilizoko baina ya mifumo husika, manufaa yake na gharama.
Demokrasia za Kikatiba
Demokrasia nyingi, lakini si zote zina msingi kwenye katiba iliyoandikwa au kwenye sheria ya juu kabisa ambayo inanuiwa kuwaongoza watunzi wa sharia na sharia ambazo wanazitunga. Katiba zilizo andikwa zinatoa hakikisho kwa wananchi kuwa serikali inaitajika kufanya kazi katika njia fulani na kutimiza haki fulani.
Nguvu za demokrasia halisi zinategemea uhuru na haki fulani za kimsingi. Uhuru na haki hizi lazima zilindwe ilikuahakikisha demokrasia itafaulu. Katika nchi nyingi haki hizi zinapatikana na kulindwa na katiba. Katiba pia huelezea miundo na kazi za serikali. Inatoa miongozo ya kuunda sharia nyinginezo. Kwa kawaida huwa inalindwa dhidi ya kufanyiwa marekebisho na vigongo wa serikali fulani kwa kuwa na kipengele spesheli kinachohitaji idadi kubwa kabla ya kipengele kubadilishwa au kuwasilisha mabadiliko yoyote kwa Wapigakura kupitia kwa kura ya maamuzi.
Mahitaji ya Kimsingi kwa nchi kuweza kuelezwa kuwa demokrasia
Kutokana na kuongozeka kwa idadi ya demokrasia zinazoandaa chaguzi huru na za haki na kujitangaza zenyewe kuwa maataifa ya kidemokrasia, seti ya mahitaji ya chini zaidi yameundwa na baadhi ya wananadharia. Chaguzi peke yake hazifanyi nchi kuwa demokrasia. Orodha ifuatayo ya mahitaji ya chini imeundwa kutokana na uchunguzi wa nchi za kidemokrasia na usomaji wa nadharia mbalimbali zinazohusu demokrasia. Inatoa mtazamo mzuri wa kijumla kuhusu maana ya demokrasia na vigezo vya kupima ikiwa nchi ni demokrasia au si demokrasia.
- uwezo wa kudhibiti maamuzi ya serikali kuhusu sera ambao kikatiba umepewa wawakilishi walochaguliwa.
- wawakilishi waliochaguliwa katika chaguzi huru na za mara kwa mara.
- wawakilishi waliochaguliwa wanatumia uwezo wao wa kikatiba bila kukabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa maafisa wasiochaguliwa.
- watu wote wazima wa haki ya kupiga kura katika chaguzi.
- watu wote wazima wana haki ya kuwania afisi ya umma.
- wananchi wana haki ya kujieleza kuhusu maswala ya kisiasa,yanayoelezwa kwa upana, bila ya hatari ya adhabu kutoka kwa serikali.
- wananchi wana haki ya kutafuta njia mbadala ya kupata maoni, kama vile vyombo vya habari, na njia zingine zinazolindwa na sharia.
- wananchi wana haki ya kuunda miungano na mashirika yanayojitegemea, pamoja na makundi spesheli na vyama vya kisiasa vinavyojitegemea.
- serikali ni huru na inaweza kufanya kazi bila ya vizuizi kutoka nje kama vile vya shinikizo za miungano na jumuiya.
Iwapo sharti lolote miongoni mwa haya halipo, wataalamu hudai kuwa nchi hiyo si demokrasia kamili.
Uhakiki wa Serikali
Kuwaelimisha wananchi kuhusu demokrasia ambamo wanaishi kuna maana kuwa waelimishaji watawapa baadhi ya vifaa vya kuchanganua hali zao. Katika hali zingine hii inaweza kuchochea ukosoaji mkubwa wa serikali, nguvu ambazo inazo, namna ambavyo inafanya kazi, na iwapo au la inaonekana kutimiza ahadi zilizotolewa wakati wa uchaguzi. Waelimishaji watataka kujiandaa kukabiliana na ukosoaji huu katika njia ya ubunifu ili wanaoelimishwa pia waweze kujifunza namna ya kukabiliana na ukosoaji wao katika njia ya kidemokrasia na amani.
Maelezo:
[1] Demokrasia kwa Wote, (Afrika Kusini: StreetLaw, 1995), 4.
[2] Ibid, p4
[3] Ibid, p4
[4] Ibid, p4
[5] Civitas, Viwango vya Kitaifa kwa raia na Serikali (Calabasas, CA: Kituo cha Elimu kwa Raia, 1994).
[6] Taasisi ya Kidemokrasia ya Namibia, Demokrasia na Wewe: Mwongozo wa Kusaidia Kuelewa Vizuri (Windhoek: n.p.), 6.
[7] ML Strom, Uraia na Demokrasia (Pretoria: Idasa, 1996), 13.
[8] Claude Ake, alinukuliwa katika Kumbukumbu za Demokrasia (Pretoria: Idasa, 1997).
[9] Bunge Kuu la Umoja wa Mataifa. 1948. Mwafaka Bia kuhusu Haki za Binadamu. Kifungu cha 217 A (III).