Uchaguzi hufanyika katika mfumo wa kisheria uliopo. Katika jamii za kimpito, mfumo huu huenda ukawa changamano zaidi, pamoja na aina mbalimbli za mipango ya muda na sheria kutoka kwa mfumo uliopita, au hata na vipengele vya sheria vya kimpito au sheria inayowezesha, kama inavyoweza kupatikana katika nchi ambazo hapo mwanzoni zilijumuisha Muungano wa Urusi na Yugoslavia, ambazo japo kwa muda, hubadilisha au hutoa ruhusa ya kukawiza sheria za awali (au vipengele vya sheria hizo). Katika hali kama hizo, amri za rais ambazo zinaathiri mchakato wa uchaguzi vilevile si ngeni.
Katika mfumo wa kisheria, kunaweza kuwa na sheria fulani mahususi au vipengele ambavyo vitaathiri shughuli za elimu kwa Wapigakura. Sheria hizi zinafaa kutambuliwa na athari zake kwa utekelezaji wa Mpango zitathminiwe.
Masharti ya Kikatiba
Hasa, katiba itafafanua masharti ya mtu kuhitimu kuwa raia na vilevile haki za uraia, ufaafu wa kupiga kura na kugombea uchaguzi, na mipangilio mingine ya uchaguzi ya kijumla. Itafafanua miundo ya serikali, na hivyo matokeo ya uchaguzi, na kutambulisha namna umma utawakilishwa na manufaa yanayotarajiwa kutokana na uwakilishi huo. Katiba vilevile huenda ikashughulikia mikakati ya kijumla ya kiusalama, majukumu ya kihuduma ya mawakala na afisi mbalimbali za serikali kwa wenyewe kwa wenyewe au kwa umma, na masuala ya ubora na usawa.
Kwa sababu chaguzi zinahusishwa kimsingi na urithi na uongozi wa kidemokrasia, sehemu kubwa ya shughuli ya uchaguzi huenda ikalindwa kikatiba. Waelimishaji wanafaa kukubali katiba, vipengele mahususi vya katiba ya nchi au serikali yao, na namna ambavyo watasimamia ujumbe na maadili ya Mpango wao wa elimu kwa Wapigakura.
Pale ambapo katiba ipo, kunaweza kuwa na aina mbalimbali za sheria zilizowekwa zinazohusiana na maadili ya wasimamizi wa uchaguzi, mipaka na mamlaka yao, na majukumu yake (tazama Sheria ya Uchaguzi).
Sheria Zingine katika Kiwango cha Kitaifa
Mbali na sheria mahususi ya uchaguzi, sheria zingine mbalimbali katika kiwango cha kitaifa nchini zinaweza kuathiri Mipango ya elimu kwa Wapigakura. Sheria hizi zinaweza kuhusisha zile sahili na vilevile zile ambazo ni tata na hii inaweza kusababisha wasiwasi. Mfano wa sheria iliyo sahili ni kama vile kuhakikisha kuwa machapisho yamesajiliwa, yanatambuliwa, na kutolewa kwa maktaba zenye kibali cha uchapishaji na Majumba ya kuhifadhi nyaraka za umma. Sheria ambazo ni changamano zaidi zinaweza kusimamia ikiwa waelimishaji wanahitaji ruhusa ya mmiliki au mtumizi wa mali inayomilikiwa kibinafsi, kama vile shamba, ili kuendesha shughuli za uelimishaji wa Wapigakura. Na wasiwasi utatokea iwapo waelimishaji wanahitajika kuwa na kibali cha kiusalama ili kuweza kuendesha elimu katika kambi ya kijeshi.
Sehemu hii inawazindua tu waelimishaji kuhusu haja ya kuchunguza sheria ambayo itakuwa na athari kwa Mpango wa elimu kwa Wapigakura. Katika hali ambapo pana uwezekano wa kutokea kwa mzozo, hukumu zitatolewa kuhusu ni vipi hasa ambavyo Mpango unaafikia masharti yote ya kisheria hata kama masharti haya yamewekwa ili kuhujumu usambazaji shwari wa habari au uelimishaji wa wananchi. Katika hali ambapo hakuna uwezekano wa kutokea kwa mzozo huu, uamuzi utafaa kufanywa kuhusu athari za kufuata sheria fulani mahususi na hivyo uwezo wa kuchukua aina fulani mahususi ya Mpango.
Kuna sehemu kadha za kawaida za sheria ambazo waelimishaji watafaa kuzingatia, zikiwemo:
- vyombo vya habari na uchapishaji
- usalama
- uchangishaji wa fedha na misaada
- uhuru wa kupata habari
- elimu na mafunzo
Sheria inaweza kuathiri namna vifaa (vya kimaandishi) vinavyochapishwa, kwa mfano, upeperushwaji ambao vyombo vya habari vinaupa mchakato wa uchaguzi, maudhui na kimo cha matangazo, na uwezo wa kupokea upeperushaji bila malipo. Sheria inaweza kuwa ilihimiza au kuhujumu wingi wa vyombo vya habari. Kutokana na hayo, hii inaweza kuathiri idadi ya vyombo vya habari, sehemu yake ya soko, hadhira yake lengwa, na kiwango ambacho vyombo hivyo vinaweza kuwa chanzo aminifu cha habari.
Tume za uchaguzi na vyama vitafaa vilevile kuzingatia vipengele vya kisheria ambavyo vinadhibiti uwezo wa kufikia nafasi ya upeperushwaji (na vyombo vya habari) bila malipo. Pia huenda kukawa na sheria ambayo inahusu namna ya kuweka wazi, hasa, mahitaji kuwa chanzo na nguvu za ujumbe wowote unaohusiana na uchaguzi au matoleo mengine, vikiwemo vifaa (vya kimaandishi) vya elimu kwa Wapigakura, vitambuliwe. Kunaweza kuwa na sharti kuwa vifaa vyote vilivyopigwa chapa vichunguzwe na serikali kabala ya kuchapishwa kwake.
Kwa habari zaidi kuhusu masuala ya aina hii, tazama Sehemu ya Mada ya Vyombo vya Habari na Chaguzi, hasa Kanuni za Kisheria, Mfumo wa Kisheria kwa Vyombo vya Habari, Sheria au Taratibu kuhusu Vyombo vya Habari wakati wa Uchaguzi, na Habari kwa Mpiga Kura
Katika baadhi ya nchi, sheria kuhusu usalama zinaweza kuwa na athari kwenye mikusanyiko ya watu, mashirika yao, uzingatiaji wa wakati, na ukuzaji. Shughuli za nyanjani zinaweza kuwekewa mipaka na amri za kutotembea. Sheria za usalama zinaweza kuwa pamoja na zile zinazowekea mipaka (labda katika sehemu ya nchi au katika nchi yote) na zile ambazo zinatoa msaada wa maana kwa uchaguzi. Katika hali kama hizi, wale wanaopanga shughuli za elimu watafaa kuelewa majukumu ambayo vitengo vya polisi na jeshi vinaweza kutekeleza katika maeneo kama vile kuelekeza au kukabiliana na umati, usaidizi kuhusu taratibu, na uwezo wa kuwafikia wafanyikazi wao wenyewe wanaohusiana na utoaji elimu kwa Wapigakura.
Ugharamiaji wa Mipango ya kielimu unahitaji usaidizi kutoka kwa serikali, mashirika, au vyanzo vingine vya kimsaada, na kibinafsi. Nchi nyingi zina sheria kuhusu uchangishaji wa pesa, utoaji wa ripoti za fedha, usajili wa maafisa wa fedha au wafanyikazi wa kuchangisha pesa, na jinsi ambavyo fedha hizi zinatozwa ushuru au zinaruhusiwa kutolipa ushuru.
Mipango ya elimu ambayo inatumika katika nchi ambazo zina sheria zinazotawala uhuru wa habari zitahitajika kutimiza au kuzingatia vipengele vya sheria hiyo. Pale ambapo sheria kuhusu uhuru wa habari haipatikani, pia itawawezesha kukuza uwazi wa serikali, ambao kila mara ni kiungo muhimu cha Mipango bora yahabari na elimu. Pale ambapo sheria yoyote kuhusu uhuru wa kutoa na kupokea habari haupatikani, au pale ambapo ni finyu, shughuli kama hizo huenda zikawa ngumu lakini sio kuwa haziwezekani.
Kwa kuwa elimu kwa Wapigakura na raia kimsingi ni shughuli za kielimu zisizo rasmi – isipokuwa pale ambapo mtalaa umeingizwa katika mfumo wa kawaida wa shule – waelimishaji huenda wasilazimike kuzingatia kikamilifu sheria ya kawaida kuhusu elimu. Lakini huenda wakatakiwa kuzingatia sheria inayohusu uandikishaji na uajiri wa waelimishaji na viwango vyovyo vya mafunzo vya kitaifa. Pamoja na hayo, huenda wakataka kutumia miongozo ya mahitaji ya mafunzo yoyote zaidi ya kitaifa.