Kwa kutegemea hali ambapo uchaguzi unafanyika, juhudi za uelimishaji wa Wapigakura zisizo na mwegemeo zinaweza kuwa rasmi, zikitekelezwa na wenye mamlaka ya kusimamia uchaguzi, au unaotekelezwa na mashirika ya kijamii pekee yao, au unaweza kuwa muungano wa yote mawili. Kuhakikisha umoja wa ujumbe, usahihi wa hoja, na umbali ambao habari zinaweza kufikia, itakuwa muhimu kwamakundi yote yanayoshiriki katika shughuli ya uelimishaji wa Wapigakura kukuza na kuendeleza uhusiano mwema.
Wenye Mamlaka ya Kusimamia Uchaguzi
Tume ya kusimamia uchaguzi inaweza kuwa na mpangilio wa aina mbalimbali. Inaweza kuwani tume ya kudumu na wanachama wa kudumu na wafanyikazi waliotaalamika. Inaweza kuwa tume ya muda iliyoanzishwa muda mfupi kabla ya uchaguzi na inayohusisha wanachama wa muda na wafanyikazi wachache. Au inaweza kuwa kitengo cha kiutawala katika idara ya kiserikali, labda na wafanyikazi walioongezewa. Katika hali yoyote ile, wenye mamalaka ya kusimamia uchaguzi watakuwa na haja ya kuhakikisha kuwa habari sahihi na zinazotolewa kwa wakati ufaao kwa Wapigakura zinasambazwa kwa wingi iwezekanavyo.
Kwa kutegemea raslimali walizonazo, wasimamizi wa uchaguzi wanaweza kuwa na uwezo wa kuendeleza Mpango wao binafsi wa elimu kwa Wapigakura. Au wanaweza kutegemea aidha kikamilifu au kwa kiasi fulani kwa usaidizi wa kimataifa na / au makundi ya kijamii kutekeleza wajibu huu. Ugawanaji wa majukumu pia unaweza kuibuka, ambapo tume ya uchaguzi inachukua wajibu wa utoaji wa elimu jumla kwa Wapigakura, kwa mfano, huku mashirika ya kimataifa na mashirika ya kijamii yakilenga makundi maalum, kama vile jamii ndogo au wanawake Wapigakura. Katika hali hii, maingiliano ya mara kwa mara, katika muundo wa ubadilishanaji na ushirikishi wa habari, litakuwa jambo la kimsingi. Mpangilio wowote ule, tume ya kusimamia uchaguzi itakuwa na haja maalum katika kusimamia Mpango rasmi wa uelimishaji wa Wapigakura. Hata hivyo, ni mojawapo njia ya kuidhihirisha mamlaka ya uchaguzi kwa umma. Wasimamizi wa uchaguzi watataka kuhakikisha kuwa habari ni sahihi na haiegemei upande wowote. Ubora wa mpango wa elimu kwa Wapigakura, katika maudhui yake na jinsi unavyotekelezwa, pia utaathiri mtazamo wa umma kuhusu ufaafu na utaalamu wa wenye mamlaka ya kusimamia uchaguzi.
Pamoja na afisi ya kitaifa, wasimamizi wa uchaguzi wanaweza kuwa na tume za mitaani au za kimaeneo ambao baadhi ya majukumu yao mapana ni kusambaza habari kwa umma, ikiwemo elimu kwa Wapigakura. Kuhakikisha kuwa kuna uhusiano wa karibu baina ya wale wenye wajibu wa kusimamia uchaguzi na wale wenye jukumu la kuwaelimisha Wapigakura katika viwango vyote ni muhimu.
Haja ya Habari Bora
Mipango ya elimu kwa Wapigakura inayofaulu inategemea habari bora au ifaayo. Habari hii inaweza kuangaliwa katika mtazamo wa mchakato wa uchaguzi na Wapigakura.
Kwanza, wale wanaowajibikia elimu kwa Wapigakura wanahitaji habari wazi, sahihi na inayotolewa kwa wakati ufaao kuhusu mchakato wa uchaguzi. Iwapo mfumo wa kisheria na wa kimpangilio uko katika hali ya wasiwasi wakati ambapo Mpango unaundwa, waelimishaji wa Wapigakura watataka kuhakikisha kuendelea kuwepo kwa njia wazi za mawasiliano na wale ambao wana jukumu la kutengeneza sheria au kutunga kanuni ili habari ziweze kupatikana haraka zaidi iwezekanavyo.
Kuhakikisha ufaafu wa Mipango ya elimu kwa Wapigakura, habari zinafaa kupatikana kuhusu Wapigakura na kutoka kwa Wapigakura wenyewe. Sifa za Wapigakura ni zipi? Je, kuna sehemu za Wapigakura, kama vile vijana na Wapigakura wa mashambani, kwa mfano, ambazo zinaonekana kuhuzunika au kutokuwa na habari sahihi? Je, nini ambacho Wapigakura wanakiona kuwa kinachokanganya au kinachotisha kuhusu mchakato wa kujisajili au wa kupiga kura? Je, kuna vipande muhimu vya habari ambavyo hawavifahamu? Je, kumekuwepo na mabadiliko kwa taratibu za kupiga kura ambazo hawazifahamu? Hizi ni aina za habari ambazo zinafaa kutolewa ili kuhakikisha kuwa Mpango wa elimu kwa Wapigakura unatosheleza mahitaji ya Wapigakura. Katika viwango mbalimbali vya Mpango wa elimu kwa Wapigakura, dhana, ujumbe, na matoleo ya vyombo vya habari yanaweza kufanyiwa majaribio kupitia kwa makundi ya utafiti au njia nyinginezo za kutafiti soko ili kutathmini uwazi na ufaafu wa habari. Inawezekana kuitisha mchango na maoni zaidi kutoka kwa Wapigakura.
Linaonekana jambo wazi na linalotarajiwa kupendekeza kuwa kuwasiliana na Wapigakura kupitia kwa Mipango ya elimu kwa Wapigakura kila mara husababisha kupatikana kwa habari bora kuhusu namna Wapigakura wanavyouona mchakato wa kupiga kura na matatizo yoyote yanayohusiana nao. Hata hivyo, wakati wa maandalizi ya uchaguzi, wasimamizi wanaweza kuonekana kupuuza chanzo hiki cha habari. Pia kuna mazoea kwa wale ambao wanashughulika na mambo ya ndani na ya kila siku ya uchaguzi kutokuwa katika hali ya kujua yale ambayo Wapigakura wa kawaida wanajua. Mpango mzuri wa elimu kwa Wapigakura, kwa hivyo, utahusisha utaratibu wa jinsi ya kupata habari kutoka kwa Wapigakura na kuzitoa kwa wasimamizi wa uchaguzi ili wazitafutie suluhu.
Idara za Serikali
Mbali na wenye mamlaka ya kusimamia uchaguzi, kuna makundi mengine ya kisheria ambayo yatahitajika kushauriwa wakati ambapo Mpango wa elimu kwa Wapigakura utakuwa unatengenezwa. Katika baadhi ya nchi, idara za habari au elimu zinaweza kuwajibikia Mipango endelevu ya elimu kwa raia. Kwa sababu elimu kwa raia ina sehemu muhimu ya ujenzi wa taifa, afisi za raisi, mashirika ya mawasiliano au utangazaji, na idara zinazohusika na maendeleo, mipango ya kikatiba, au shughuli zingine za kitaasisi zinaweza pia kuhusika. Katika kila mojawapo wa makundi haya, kunaweza kuwa na wataalamu ambao wana maoni kuhusu shughuli za elimu kwa Wapigakura, jinsi ambavyo shughuli hizi zinaweza kuendelezwa, na kiasi ambacho zinakamilishana au kushindana katika Mipango yao ya elimu kwa raia.
Idara za elimu zinaweza kuhusika kimsingi na watoto, lakini mara nyingi pia zinahusika na elimu na mafunzo kwa watu wazima. Na pia zinaweza kuwajibikia mifumo ya utoaji leseni na kukadiria kufuzu kwa wale ambao wanafanyakazi ya kielimu. Au zinaweza kukuzwa, na hivyo, kuwa mojawapo wa washika dau, katika harakati za kupima kufuzu kwa watu na utoaji mafunzo au mabaraza ya kutekeleza shughuli hizi. Hawa ni washiriki muhimu, na vilevile washindani watarajiwa, hasa iwapo bajeti zao binafsi hazitoshi.
Makundi Huru ya Kisheria
Makundi mengine huru ya kisheria yanaweza kuwajibikia kusimamia sehemu mahususi za katiba ya nchi. Tume za Haki za Kibinadamu, kwa mfano, mahakama za kikatiba, tume zinazowajibikia usawa wa kijinsia na kijamii, na mabaraza yanayohusika na makundi spesheli yote yamekuwa na ongezeko la majukumu ya uhamasishaji na ya kielimu. Kwa hivyo, yana jukumu la kutekeleza wakati wa uchaguzi na yanafaa kushiriki katika majadiliano na ushirikishi wa Mpango wa elimu kwa Wapigakura.