Katika nchi, kunaweza kuwa na seti ya sheria na/au amri ambazo zitaathiri shughuli za uelimishaji wa wananchi hata kama zikiendeshwa na au mashirika ya kimataifa. Mara nyingi, maafisa wa nchini watafuata amri zinazotawala shughuli kama vile mihadhara ya umma (ruhusa maalum, katika muundo wa kibali, kwa mfano, inaweza kuhitajika) na inayosawazisha pale ambapo vifaa vya uchaguzi, kama vile mabandiko, vinaweza kubandikwa na pia ni nani anayewajibikia utoaji wake mahala vilipobandikwa. Amri zinazotawala viwango vya kelele na usumbufu wa umma pia zinaweza kutumika. Kufeli kwa wale ambao wanaendesha uchaguzi kuzifahamu na kuzingatia amri hizo za nchini kunaweza kusababisha faini na adhabu katika kiwango cha nchi.
Uchambuzi huu wa sheria haujitoshelezi na hauzingatii sheria za kawaida na kimsingi za nchi na sheria zao za wafanyikazi, baiashara, na haki za kijamii. Mipango ya elimu kwa Wapigakura na elimu kwa raia zote hupatikana nje ya sheria za kitaifa kwa sababu tu kuwa zinahusika na uchaguzi au masuala mapana ya kisiasa, kijamii, au kiuchumi. Waelimishaji watafaa kuelewa na waweze kuzingatia sheria za nchi pale mbapo zinatumika. Hii inaweza kufanya majukumu ya mashirika ya kimataifa yanayosaidia katika kutoa elimu kwa Wapigakura kuwa ngumu. Kwa sababu hii, uundaji wa ushirikiano na mashirika ya kienyeji au chini ya uangalizi wa utawala wa kusimamia uchaguzi, mara nyingi huwa muhimu.
Sheria za Uchaguzi
Sheria za uchaguzi zinaweza kuwepo kama fungu la sheria tofauti au kama mkusanyiko mmoja wa sheria. Sheria katika sehemu hii zinaweza kuzungumzia mfumo wa uchaguzi, haki za kupiga kura, uundaji na utendakazi wa usimamizi wa uchaguzi, usajili wa Wapigakura, uandalizi wa uchaguzi, na ufadhili wa kampeni. Ingawa waelimishaji wa Wapigakura huenda wasishiriki katika utungaji wa sheria hii, itakuwa na athari kubwa kwa shughuli ya elimu kwa Wapigakura.
Mifumo ya Uchaguzi
Mifumo tofauti ya uchaguzi hutoa matarajio tofauti kwa Wapigakura na wasimamizi wa uchaguzi. Uteuzi wa mfumo fulani wa uchaguzi huashiria hali za kijamii ambamo Wapigakura wanajipata. Kama sheria haiwezi kufanyiwa marekebisho kwa njia rahisi, kunaweza kuwa na nyakati ambapo mabadiliko ya kijamii hutangulia mabadiliko katika sheria ya uchaguzi. Hii inaweza kusababisha kutokuwepo kwa ufungamano baina ya Wapigakura na mfumo. Hivi maajuzi baadhi ya nchi zimeshiriki katika mijadala kuhusu mabadiliko yafaayo katika mifumo yao ya uchaguzi. Hali na uzingatiaji wa wakati mwafaka katika kufanya mabadiliko kwa mfumo wa uchaguzi kutakuwa na athari kuu kwa Wapigakura. Pale ambapo mfumo umekuwa ukitumika kwa wakati fulani, kunaweza kuwa na uchukulio fulani kuwa huu ndio mfumo wa pekee ulio mzuri, na hivyo kutakuwepo upinzani kwa mabadiliko.
Kimsingi, hata hivyo, waelimishaji wa Wapigakura watataka kupigia debe mifumo ambayo inapunguza uchangamano katika kiwango cha kupiga kura na kuamua matokeo. Kwani ni uwezo wa kuelewa uhusiano baina ya kura yao na matokeo ya uchaguzi ambayo hutoa ushawishi muhimu kwa Wapigakura kushiriki.
Sheria za Uchaguzi na Elimu kwa Wapigakura
Wajibu wa kisheria wa elimu kwa Wapigakura huwa mara nyingi mahitaji ya awali ya kuweza kupata bajeti na wafanyikazi wa kusaidia Mpango. Kwa kuzingatia kiwango cha ugatuzi wa utawala wa uchaguzi, wajibu wa kisheria unaweza kuibuka kutoka kwa aidha sheria za kitaifa au za serikali. Wakati huo huo, kunaweza kuwa na nchi ambapo sheria zinatenga shughuli pana za elimu kwa Wapigakura kutoka kwa wasimamizi wa uchaguzi: Spain ni mfano mmoja. Katika hali kama hizi, wasimamizi wa uchaguzi wanafaa kutoa habari kwa Wapigakura katika miongozo finu sana.
Kwa upande mwingine, uelewa zaidi wa umuhimu wa elimu umesababisha kuwepo kwa vipengele vya elimu kwa Wapigakura vyenye maelezo ya kina sana katika sheria ya uchaguzi. Katika baadhi ya hali, hii imehusishwa na habari kwa umma na sheria ya kampeni. Sheria mara nyingi zinafaa kufasiriwa kwa uangalifu, hata hivyo, na uhuru wa mamlaka ya kusimamia uchaguzi, kipindi chao ofisini, na kusimamia bajeti zao, yote yana athari kwa uwezo wao wa kuanzisha Mipango bunifu ya habari kwa umma na elimu kwa Wapigakura.
Vipengele vya kisheria vinaweza kuwa sahili na pia changamano. Katika baadhi ya hali, majukumu ambayo hutengewa wasimamizi wa uchaguzi huenda yasiwe wazi katka kuwajibisha elimu kwa Wapigakura. Sadfa iliyopo baina ya uchaguzi na demokrasia, kwa mfano, inaweza kusababisha wasimamizi wa uchaguzi kupokea wajibu wazi wa kuendesha elimu kwa Wapigakura au kuifasiri kutokana na majukumu yao.
Katika nchi ya Ethiopia, uchaguzi wa kundi la kufanyia marekebisho katiba ulihitaji kuanzishwa kwa baraza la uchaguzi. Pamoja na “mamlaka na majukumu” mengine, baraza la uchaguzi linahitajika kutoa elimu kwa raia kwa wingi kuhusiana na uchaguzi.
[1]
Kipengele sawia kinapatikana katika Sheria ya Uchaguzi ya Jumuia ya Madola ya Australia ya 1918. Majukumu ya tume ya uchaguzi ni “kukuza uelewa wa umma kuhusu masuala ya uchaguzi na bunge kupitia kwa mipango ya habari na elimu na njia zinginezo.” [2] Maarifa, hata hivyo, hayana mipaka ya ubunifu. Katika Australia, hali ya lazima ya upigaji kura imesababisha waelimishaji wa Wapigakura kufanya ufasiri mpana wa wajibu wao. Katika kutekeleza wajibu wao wa kuhakikisha kuwa Wapigakura wote wanaweza kupiga kura zao na kuelewa umuhimu wake, serikali inawacha jukumu la kupiga kura kwa Wapigakura wenyewe. Matokeo yamekuwa ni Mpango mpana wa elimu kwa Wapigakura.
Katika nchi ya Kanada, wajibu wa kiuchaguzi umepanuliwa katika njia ya kuvutia kuhakikisha kuwa elimu inatolewa katika hali jumuishi zaidi. “Afisa Mkuu wa Uchaguzi anaweza kuendeleza Mipango ya elimu na habari ili kufanya mchakato wa uchaguzi kujulikana vizuri zaidi na umma, hasa watu wale au makundi ya watu wanaoweza kupata matatizo katika kutekeleza haki yao ya kidemokrasia.” [3] Huu ni mfano mzuri zaidi wa namna ambavyo mabadiliko katika muktadha wa kijamii yamefuatiwa na maagizo ya kisheria.
Kwa bahati mbaya, hali haiwi hivi kila mara. Katika hali mbili za kimpito, utawala wa muda umepewa vilevile maagizo mafupi. Katika kura ya maamuzi kuhusu uundaji wa nchi ya Eritrea, mkataba unasema kuwa utawala wa kusimamia uchaguzi una kama mojawapo wa majukumu yake “kuhamasisha watu kuhusu kura ya maamuzi na kuwapa Wapigakura habari.” [4] Na katika nchi ya Bosnia na Herzogovina, sehemu ya mkataba inasoma, “Ili kuwafahamisha wananchi wa Bosnia na Herzegovina kuhusu mchakato wa uchaguzi na haki za wananchi kama Wapigakura, Tume ya Muda ya Uchaguzi imeamua kuwa vituo vyote vya redio na runinga kote Bosnia na Herzegovina na katika nchi zote mbili itatangaza vifaa vya kielimu kuhusu elimu kwa Wapigakura ambavyo vimetolewa na Tume ya Uchaguzi ya Muda.” [5]
Hii inatoa dhihirisho la uhusiano wa karibu mno baina ya elimu kwa Wapigakura na jukumu la kijumla la vyombo vya habari katika uchaguzi. Na kwa kusambaa kila mahali kama yalivyo makala yanayohusu vyama kutumia vyombo vya habari, pia inadhihirisha uhusiano wa karibu baina ya elimu kwa Wapigakura na propaganda za kisiasa.
Sheria ya Uchaguzi ya Mozambique ina sura yenye mada “Propaganda ya Uchaguzi na Elimu kwa Wapigakura”. Katika sura hiyo yenye vifungu kumi na moja, kimoja tu, Kifungu 102 (Elimu kwa Raia), inahusiana na masuala halisi ya elimu kwa Wapigakura. Lakini kwa kuunganisha sehemu hizi, inaonekana kuwa Wapigakura wanaweza kuwa sio tu wenye ufahamu bora, lakini wenye makini zaidi katika kushiriki katika masuala ya uchaguzi kama watafahamishwa kuhusu kampeni iliyowekwa wazi zaidi na kwa habari kwa Wapigakura ifaayo.
Sheria ya Mozambiki inatoa maelezo kadha zaidi kuhusu ujumbe na mbinu za habari na elimu kwa mpiga kura:
- Kupitia kwa vyombo vya habari, Tume ya Uchaguzi ya Kitaifa itaendeleza elimu kwa wananchi kuhusu malengo ya uchaguzi, mchakato wa uchaguzi, na namna mpiga kura anavyopiga kura yake.
- Taarifa za pamoja, taarifa zisizorasmi, na sheria zingine za Tume ya Uchaguzi ya Kitaifa zitachapishwa na kitengo cha umma cha vyombo vya habari bila malipo na kama jambo la muhimu. [6]
Zaidi ya sheria wastani za uchaguzi, sheria za kibinafsi kuhusu haki za upigaji kura, kama zile zilizo Marekeni na Urusi, zinaweza kuhitaji kuwa wasimamizi wa uchaguzi katika viwango vyote watoe habari na elimu kwa Wapigakura wote au kwa makundi fulani lengwa na kufanya mchakato wa upigaji kura kuweza kufikiwa zaidi, kwa mfano kwa Wapigakura wenye upungufu au kwa wale wanaopiga kura kwa mara ya kwanza.
Katika baadhi ya hali, mara nyingi katika mazingira ya kimpito, sheria za uchaguzi hazisemi chochote kuhusu suala la kuwafahamisha Wapigakura. Katika hali hizi, wasimamizi wa uchaguzi wanafaa kuamua ikiwa au la wana mamlaka ya kuendesha elimu kwa Wapigakura kama sehemu ya maandalizi yao mapana ya uchaguzi. Uamuzi huu unaweza kuathiriwa na muktadha wa kijamii na kisiasa ambamo uchaguzi unafanyika, taratibu za kisheria (kwa mfano ni kwa njia ganivipengele vya kisheria vinafaa kufasiriwa), na masuala mengine muhimu kuhusu wajibu wao. Je, umma unatarajia wasimamizi wa uchaguzi kutoa maelezo ya kimsingi kuhusu uchaguzi? Kuna pesa za kufanya hivyo? Washiriki wa kisiasa watachukulia hili kuwa nje zaidi ya wajibu wa mamlaka ya wasimamizi wa uchaguzi? Je, uchukulio huu utaathiri uhalali wa taasisi au wa uchaguzi? Masuala kama haya, pale mbapo wajibu wa kisheria unakosekana, yamesababisha Tume ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Montenegro, kwa mfano, kutoshiriki katika shughuli za uelimishaji wa Wapigakura.
Pia katika nchi ambazo zinapitia mabadiliko, ni jambo la kawaida kupata hali ambapo wasimamizi wa uchaguzi wanawajibu wa kisheria wa kuwafahamisha Wapigakura, lakini hawajatengewa mgao wa bajeti wa kuwawezesha kutekeleza majukumu haya. Hii inajulikana kama wajibu usiofadhiliwa. Katika mazingira ambapo raslimali ni haba, shughuli ya upigaji kura itamaliza fedha zote zilizopo. Mara nyingi, elimu kwa Wapigakura huwa inapewa uzingatifu wa chini au inachukuliwa kuwa starehe. Nchi ya Georgia inatoa mfano mmoja ambapo bajeti za uchaguzi kila mara zimepewa fedha zisizotosha, na utoaji wafedha za serikali hufanyika baada ya kuchelewa katika mchakato wa uchaguzi. Katika hali kama hizi, jamii ya kimataifa mara nyingi hushirikishwa, na kuchukua gharama za juhudi za uelimishaji wa Wapigakura.
Sheria za Uchaguzi na Ukuzaji wa Demokrasia
Kwa sababu ya umuhimu wa uchaguzi katika kutunza demokrasia na taasisi zake, wasimamizi wengi wa uchaguzi wametumia mamlaka waliyopewa kwa kuwafahamisha umma na kuelimisha Wapigakura kupanua kazi yao hadi kwa shule na taasisi zingine za kielimu. Katika baadhi ya hali, kazi ya aina hii inaweza kutochukuliwa kama elimu kwa raia katika ukamilifu bali inaweza kuchukuliwa zaidi kama elimu kwa au kuhusu uchaguzi. Urusi na Ukraine ni mifano miwili ambapo wasimamizi wa uchaguzi na waelimishaji wamefanya juhudi za pamoja kuanzisha kozi za madarasni kuhusu uchaguzi.
Kuna nyakati, hata hivyo, ambapo mienendo ya uchaguzi inaonekana kwenda zaidi ya aina hii ya elimu kwa Wapigakura na hulazimisha wasimamizi wa uchaguzi kuingilia katika kiwango cha ndani zaidi. Katika nchi ya Mexico, mwenendo huu unahitaji Taasisi Shirikishi ya Uchaguzi “kusaidia katika uendelezaji na usambazaji wa utamaduni wa kisiasa” na “kuchangia katika ukuzaji wa maisha ya kidemokrasia.”
[7]
Hii imesababisha Mpango mpana zaidi wa kielimu ambao sio endelevu tu lakini pia unaendelea zaidi ya mipaka ya uchaguzi fulani mahususi.
Nchini Afrika Kusini, sheria ambayo inaweka msingi wa tume ya uchaguzi inaorodhesha majukumu mbalimbali ili “kukuza hali ambazo ni shwari kwa uchaguzi huru na wa haki” na kukuza “maarifa ya michakato ya uchaguzi bora na wa kidemokrasia”.
[8]Malengo ya Tume hiyo ni “kuimarisha Demokrasia ya Kikatiba”.
[9]
Hii inaweza kuwa na athari za kielimu ambazo hazikutarajiwa na tume.
Mianya ambayo imewachwa na vipengele kama hivyo, hata hivyo, inaipa jukumu kuu wasimamizi wa uchaguzi. Kwa upande mwingine, hii huenda isiwe hali ilivyo katika jamii ambapo kuna taasisi nyingi ambazo zinashindana, za kibinafsi na za umma, au pale amabapo usimamizi una lengo la kiusimamizilinalohitaji juhudi nyingi. Pia huenda isiwezekane katika jamii ambapo hakuna tume ya kudumu ya kusimamia uchaguzi. Pia ukubwa au udogo wa uchaguzi au upungufu wakifedha unaosababishwa na gharama za uchaguzi zinaweza kuifanya kuwa vigumu kwa wasimamizi wa uchaguzi kushiriki katika kitu kingine zaidi ya habari sahili kwa Wapigakura. Kwa hakika, kuendeleza Mpango wa kielimu wa kawaida badala ya Mpango fanifu wa utoaji habari kwa Wapigakura kwa kila uchaguzi unaweza kuwa ghali.
Kanuni za Uchaguzi
Kanuni za uchaguzi zinaweza, au huenda zisiweze, kuwapa uwezo wasimamizi wa uchaguzi, au vitengo vingine vya serikali, kutunga sheria zinazotawala mchakato wa kupiga kura. Sheria hufanya kazi ya kufafanua au kutoa mwanga kwa sheria za uchaguzi na kutoa mwongozo au kuelekeza wasimamizi wa uchaguzi na washirika katika mchakato wa uchaguzi. Sheria zinaweza kuelezea kuhusu masuala kama vile makataa yanayohusu kampeni au shughuli nyinginezo za kiuchaguzi, uteuzi au taratibu za kuripoti fedha za kampeni, utoaji wa masaa ya hewani ya bure, maandalizi ya mahali pa kupigia kura, uelekezaji wa Wapigakura katika siku ya kupiga kura, utaratibu wa kuamua ikiwa kura inafaa au haifai, na taratibu za kuhesabu kura. Wakati mwingine, kanuni hizi zinaweza kufanana na misitu ambapo Wapigakura na waelimishaji wanaweza kupotelea au, katika baadhi ya hali, hata kutatizwa na vichaka vya kikanuni.
Mpangilio wa wakati
Kanuni mara nyingi hufuata sheria. Hata hivyo kanuni hizi zinaweza kuwa na maelezo ya kina ambayo waelimishaji wanahitaji ili kuboresha sehemu muhimu za Mipango yao. Ikiwa waelimishaji wanapanga kuwafahamisha Wapigakura kuhusu wanachofaa kutarajia siku ya uchaguzi, kwa mfano, watahitaji ufahamu wa kina wa taratibu za mahali pa kupigia kura. Maelezo haya yanaweza kutolewa kupitia kwa kanuni na wala sio kupitia kwa sheria. Ikiwa kanuni zitazingatiwa baada ya kuchelewa katika kampeni za uchaguzi, au zinabadilishwa kwa mfululizo, muda uliopo kwa waelimishaji kuunda Mipango unakuwa finyu. Katika miktadha mingi ya kimpito, pale ambapo sheria yenyewe ya uchaguzi iko katika hali ya mfululizo wa mabadiliko katika kipindi kinachotangulia, au hata katika kipindi chenyewe cha kampeni za uchaguzi, uwezekano kuwa kanuni zinaweza kufuatwa katika wakati ufaao ili kutoa ufafanuzi ufaao ni mdogo.
Nchi ya Georgia wakati wa kampeni ya uchaguzi ya mwaka wa 2000 unatoa mfano wa hali hii. Katika majuma ya mwisho ya kampeni ya uchaguzi, bunge lilikuwa bado linajadili mabadiliko yafaayo kwa baadhi ya sheria zinazo simamia uchaguzi. Kutokana na hayo, haikuwa wazi ni toleo lipi la sheria zinazohusu uchaguzi zilizofaa kutumika. Katika hali kama hizi, ilikuwa haiwezekani kabisa kutoa kanuni kwa madhumuni ya kufafanua. Je, kanuni kama hizi zitakuwa na msingi upi? Miongoni mwa maelezo ya kina yaliyofaa kuamuliwa yalikuwa: ni aina gani za utambulishi zitakubalika katika siku ya uchaguzi? Ni njia zipi zilizofaa katika kutia alama kwenye karatasi la kupigia kura? Haya ni aina ya maelezo ya kina ambayo yanafaa kuzungumziwa na waelimishaji katika wakati ufaao.
Hata kama sheria ya uchaguzi ni dhabiti, hoja kama vile kampeni fupi ya uchaguzi, raslimali finyu za kuendeshea uchaguzi na kutokuwepo kwa mamlaka ya kudumu ya kusimamia uchaguzi zinaweza kuungana na kusababisha hali ambapo kalenda ya uchaguzi inakuja kabla ya kanuni zifaazo au muhimu. Katika hali za aina hii, kuna hatari kubwa kwa waelimishaji. Ikiwa kanuni zinafuatwa au kubadilishwa baada ya Mpango wa elimu kwa Wapigakura umeanzishwa rasmi matokeo yanaweza kuwa mkanganyiko katika siku ya uchaguzi – kinyume kabisa cha yale yaliyodhamiriwa katika Mpango.
Maelezo ya kina
Mara nyingi, kanuni zinaundwa zaidi kwa minajili ya Wapigakura kama ilivyo kwa wale wanaosimamia na wale wanaoshindania uchaguzi. Hata hivyo maelezo fulani ya kina yanaweza kuathiri ushiriki wa Wapigakura katika mchakato. Kama tokeo la vipengele vya kisheria visivyo vikamilifu au mafunzo finyu kwa wafanyikazi wa uchaguzi, kanuni zinaweza kuwa za kina zaidi. Wakati mwingine kanuni za kina zinaweza kutatiza waelimishaji ambao wana matatizo katika kuzungumzia kanuni hizi katika Mipango yao. Maelezo ya kina au hali ya juu yanaweza kuwa magumu kuyahusisha katika ujumbe wa moja kwa moja na mfupi ambao umeundwa kwa minajili ya televisheni, redio au mabango. Maaamuzi yatahitajika kufanywa kuhusu ni aina zipi za vyombo vya habari na miundo ambazo zinaweza kuhusisha habari za kina zaidi. Pia kutakuwa na shauku kuhusu kupotea au uwazi au dhamira katika hali ya kuwepo kwa habari nyingi za kiufundi. Kwa baadhi ya Wapigakura ambao hawana ufahamu au hawana uhakika kuhusu mchakato wa kupiga kura, hata hivyo, kunaweza kuwa na haja ya habari zaidi na wala sio chache. Utambuaji na ulengaji wa makundi haya ya Wapigakura utasaidia katika kuelekeza habari za kina zaidi kwa wale ambao wanazihitaji.
Mamlaka
Wakati ambapo matumizi ya kanuni za kina yanaweza kufanya kazi ya waelimishaji kuwa ngumu zaidi, kutokuwepo kwa kanuni kunaweza kuwa tatizo. Katika baadhi ya miktadha ya kimpito, wasimamizi wa uchaguzi au mabaraza mengine ya kiserikali yanayowajibika yanaweza kupewa mamlaka ya kisheria kuendeleza kanuni. Hali hii inaweza kutatiza. Ikiwa kuna mianya katika searia au zinakanganya, au hata zinakinzana, vipengele za kisheria, wasimamizi wa uchaguzi wanaweza kukosa uwezo wa kuleta uwazi au umoja katika mchakato wa uchaguzi. Bila shaka, wasimamizi na waelimshaji wanaweza kuwa na baadhi ya maswali sawa kama yale ya Wapigakura kuhusu namna ambavyo mchakato unafaa kufanya kazi. Ikiwa maswali haya hayawezi kujibiwa katika hali ya wakati ufaao, mpango wa elimukwa Wapigakura hautakuwa kamilifu na kuchanganyikiwa kwa Wapigakura kunawezekana kuendelea.
Jukumu la Mwelimishaji
Waelimishaji watataka kuchunguza kanuni zote zilizopo kwa makini na kuhakikisha kuwa wanapata kanuni hizo katika miundo ya mswada na katika muundo kamilifu (bila ya kuchukulia mmoja kuwa mwingine). Katika mswada, waelimishaji watataka kutoa maoni kuhusu namna kanuni zinaweza kuathiri kazi yao ya kielimu. Katika toleo kamilifu, waelimishaji watatumia mipango ya kielimu kuwasilisha maelezo ya kina kuhusu kanuni kwa njia iliyo sawa, na, ikiwezekana, wanaweza pia kuzingatia njia za kuwaelimisha tena wale ambao tayari wamepitia katika mpango wa awali. Labda muhimu zaidi, waelimishaji wanaweza kusihi uchapishaji wa kanuni zote na za mwisho mapema iwezekanavyo na mamlaka ya kusimamia uchaguzi kuzifuata kikamilifu hata kama kuna ushawishi wa kutenda kinyume na haya.
Upungufu wa Kisheria
Katika baadhi ya hali, elimu kwa Wapigakura inaweza kuanzishwa kirasmi katika hali ambapo hakuna sheria kamilifu. Hali ya kutokuwepo na sheria kamilifu inaweza kuathiri elimu kwa Wapigakura katika hali mbili. Kwanza, sheria ya uchaguzi inaweza kuwa kimya kuhusu jukumu la wasimamizi wa uchaguzi na vitengo vingine katika uendeshaji wa shughuli za elimu kwa Wapigakura. Na kunaweza kuwa na utata wa kisiasa na au kiuchumi ikiwa wataamua kuendelea na uelimishaji wa Wapigakura bila ya kuwepo kwa wajibu wa kisheria. Mashirika mengine yanaweza kuwa na hiari ya kutumia rasilimali kwa mipango ya elimu kwa Wapigakura ambayo inaweza kufanya mipango isiyofaa na hitilafu zisizotarajiwa kati ya matarajio ya waelimishaji na malengo ya watunzi wa sheria.
Pili, kunaweza kuwa na mianya katika sheria kuhusu masuala ya kimsingi ya mchakato wa uchaguzi ambayo yanafaa kutolewa kwa Wapigakura. Je, sheria inazungumzia masuala kama haya kwa ukamilifu na uwazi, kwa mfano, masuala kama vile: taratibu za usajili wa Wapigakura, aina za vitambulisho vinavyohitajika siku ya kupiga kura; mchakato na makataa ya kuwasilisha malalamishi; nafasi za kupiga kura mapema, kupitia kwa sanduku la kupigia kura la kutangatanga au katika hali ya kutokuwepo kwa karatasi ya kupigia kura; njia mwafaka ya kutia alama kwenye karatasi ya kupigia kura: na taratipu za kupiga kura katika siku ya uchaguzi? Na kama sivyo, itakuwa vigumu zaidi kwa waelimishaji kuzungumzia maswali kuhusu mchakato.
Ingawa mianya ya kisheria haifurahiwi, huwa inatokea. Kungojea mianya hii ijazwe huenda kusiwezekane. Upangaji wa elimu huchukua muda. Na ikiwa yametengewa muda mchache, gharama zitakuwa za juu, bila ya kutaja hatari za kupoteza rasilimali na kuwakanganya umma.
Uepukaji wa Mianya ya Kisheria
Katika hali ambapo hakuna sheria, au angalau vipengele vya kisheria, vinavyohusu elimu kwa Wapigakura, hatua zinaweza kuchukuliwa kuhakikisha kwamba Mipango haibadiliki na kuwa maelezo ya kawaida, yasiyo na manufaa, au taarifa zisizo za ukweli na zinazopotosha.
Kwanza, waelimishaji wanafaa kuwa wazi katika uelewa wao wa lengo lao, kulikariri kila mara, na kuhakikisha uaminifu kwake.
Pia inaweza kuwa muhimu kuzingatia muktadha ambamo sheria ilianzishwa au kufanyiwa marekebisho. Katika misingi ipi ya matatizo ya kiwakati na misukumo ya kisiasa mahakama yalikuwa yakitekelezea wajibu wake? Ni nini iliyokuwa sababu ya vipengele mbalimbali na vilevile vibadala ambavyo mwishowe havikuchukuliwa? Je, kutakuwepo na nafasi ya mabadiliko zaidi siku za baadaye? Ni vizuizi vipi ambavyo vinaweza kuzuia mabadiliko? Kufanya tathmini kama hii kunaweza kusaidia waelimishaji kuelewa vizuri zaidi kile kinachowezekana katika wakati huo na kupangia maisha ya baadaye.
Ingawa waelimishaji hawataweza kufafanua kila suala katika uchaguzi fulani, bado itawezekana kuwasilisha kanuni na habari muhimu. Inawezekana, kwa mfano, kusema ikiwa Wapigakura watahitajika kutoa hati za kujitambulisha, kadi za kupigia kura, au ikiwa vidole vyao vitatiwa alama na wino usioweza kufutika kwa urahisi. Lakini inawezekana kuelezea ni kwa nini kusiwe na kupiga kura zaidi ya mara moja na njia za kuzuia haya.
Wape uwezo na uwahimize washiriki mapema katika Mpango kutafuta habari kutoka kwa wao wenyewe. Orodha ya anwani, vifaa (vya kimaandishi) vyenye maelezo ya kimsingi, na mitandao ni raslimali muhimu sana kwa shughuli hii. Wale wanaohusishwa wanafaa kufunzwa kujua kuandika na kusoma na kuelewa sheria za kimsingi ili kuifuatilia wakati ambapo itapatikana au katika mchakato wote wa marekebisho.
Kuna jukumu la kielimu na uhamasishaji ambalo linaweza kutekelezwa na waelimishaji, katika utawala wa uchaguzi au katika mashirika ya kupigania haki za kijamii, pamoja na watengenezaji wa sera za umma na watunzi wa sheria. Wakati mwingine ni muhimu kufafanua au kutilia mkazo namna ambavyo mianya yote katika sheria na Wapigakura wasiofahamishwa na waliokanganyikiwa wanaweza kuathiri ubora, umoja na uhalali wa mchakato wa uchaguzi. Dhihirisha namna ambavyo matatizo yaliyopita yangeweza kuepukwa kupitia kwa sheria bora pamoja na elimu toshelevu kwa Wapigakura.
Umuhimu wa Uwazi
Uwezo wa waelimishaji, miongoni mwa wengine, kufuata matumizi ya sheria mpya, kufuatilia marekebisho kwa sheria zilizopo, au kuwa na mchango katika mchakato wa kufanyia marekebisho mfumo wa uchaguzi utategemea, kwa kiasi kikubwa, na uwezo wao wa kufikia habari na watengenezaji wa uamuzi. Ikiwa mijadala ya bunge kuhusu marekebisho ya kiuchaguizi si wazi kwa umma, ikwa hakuna notisi kwa umma na kipindi cha mjadala, ikiwa vielelezo au hata matoleo ya safi ya sheria hayatolewi au kuwekwa wazi na kuweza kufikiwa na umma, itakuwa vigumu kuendeleza elimu kwa umma katika wakati ufaao na kwa njia nzuri. Katika baadhi ya miktadha ya kimpito na ya baada ya mzozo, pale ambapo kuna mabadiliko ya dakika za mwisho kwa sheria za uchaguzi, pale ambapo kuna ufinyu wa rasilimali na mitandao ya kutoa nakala na kusambaza, na pale ambapo hakuna msingi wa kisheria au wa kisiasa utamaduni wa kisiasa kuhusu uwekaji wazi, si jambo geni kupata wasimamizi na waelimishaji wakifanya kazi bila ya toleo la mwisho la sheria. Ukuzaji wa uwazi unahitaji kuwa sehemu muhimu ya mchakato wa mabadiliko ya kiuchaguzi wakati ambapo nchi zinasonga kuelekea kwenye mifumo ya uongozi ya kidemokrasia zaidi.
Maelezo:
[1] Serikali ya Mpito ya Ethiopia, Negarit Gazeta of the Transitional Government of Ethiopia, tafsiri rasmi, Nambari 56, Agosti 23, 1993 – Nambari ya ilani 64 / 1993, Sheria za Uchaguzi za Etiopia, 5.1 (d).
[2] Serikali ya Australia, Commonwealth Electoral Act 1918, Nambari ya chapisho 7, Sehemu (1)(c).
[3] Serikali ya Kanada, Kanada Elections Act, Sheria ya Kura ya Maamuzi, Nakala Kielezo, Sehemu II, 8 (2).
[4] Serikali ya Muda ya Eritrea, Nambari ya chapisho 22 / 1992, Sura 1, 5 (1)(d).
[5] Misheni ya OSCE katika Bosnia na Herzegovina, Tume ya Muda ya uchaguzi, Sheria naKanuni, Makala 116.
[6] Serikali ya Mozambiki, Electoral Law of Mocambique,Tafsiri ya Kiingereza, Sehemu ya IV, Sura ya II, Makala 102, (1) na (2).
[7] Taasisi ya Uchaguzi ya Muungano, Federal Code of Electoral Institutions and Procedures, Kitabu cha tatu, Makala 69, 1(g) na 1(a), mtawalia.
[8] Jamhuri ya Afrika Kusini, Nambari 51 ya 1996: Sheria ya Tume ya Uchaguzi, 1996,Ofisi ya Rais, Nambari. 1602. Oktoba 1996, Sura ya 2, 5. (1) na (d). tazama http: // www.polity. org.za/govdocs/legislation/1996/act96-051.html
[9] Kama hapo juu. Sura 2, 4 tazama http://www.polity.org.za/govdocs/legislation/1996/act96;051.html