Kabla ya kwenda nyanjani pamoja na watafiti, kila hojaji inastahili kufanyiwa majaribio kwa walengwa wa kimajaribio. Walengwa wa kimajaribio wako kama wale watakaofanyiwa mahojiano wakati wa utafiti halisi. Kwa misingi hii ya kimajaribio, dosari zinazoweza kuwepo kwenye hojaji zitatambuliwa na kurekebishwa mapema.
Tafiti nyingi za kimajaribio hufanywa kwenye chumba kidogo chenye upenyu unaomwezesha mtafiti kuchunguza mahojiano halisi. Hapa mtafiti huweza kuona hasa kinachoendelea kuhusiana na maswali, majibu na ishara za kimwili kutoka kwa wahojiwa hata ingawa kwa upande mwingine huenda jambo hili likaonekana la kiorwell hali ambapo tabia na fikra za watu zinadhibitiwa.
Hali hii hutoa fursa nzuri ya kuchunguza iwapo:
- Maelekezo yanaeleweka vizuri kwa mtafiti;
- Maswali yanaeleweka vizuri kwa mtafiti na mhojiwa;
- Maswali yanasomeka vizuri;
- Maswali humweka mtu katika hali ya wasiwasi na kutostarehe;
- Wahojiwa huchoka na kutoa mawazo finyu katika majibu yao, na hasa hali hii hutokea wakati gani;
- Maswali hufumbata aina ya majibu yenye manufaa kwa watafiti.
Katika kuuliza maswali ya kimajaribio yanayohusiana na masuala ya kijamii, kulingana na maoni ya Idasa, alibainisha kuwa baadhi ya maswali kama vile, “Je, wewe hujiitaje?” huibua majibu ya sifa za kibinafsi kama vile, “mtu mzuri” na “aliye tayari kupokea mawaidha” ambao sio ujumbe unaotafutwa. Kutokana na na majibu kama haya, ilikuwa vyema kuwezesha muktadha fulani ambao mtu angejibu maswali. Hivyo swali lilibadilishwa na kuwa: “Je, katika makundi yote ya Afrika Kusini (ambapo orodha ya makundi mbalimbali ilitolewa), wewe unapatikana katika kundi lipi?”
Maswali ya kimajaribio humwongoza mtafiti kuchunguza tena baadhi ya maswali, na hata kuyaondoa maswali mengine. Iwapo kutokana na maswali ya kimajaribio itajitokeza kwamba hojaji ni ndefu sana, patahitajika wazo la kurejelea tena hojaji nzima. Maamuzi fulani yataafikiwa kwenye uchambuzi wa mwisho wa hojaji. Iwapo wazo lote la hojaji litahitajika kutatupiliwa mbali katika utafiti hata ingawa huenda ukawa ni wa kuvutia lakini hauna maana au kutupilia mbali tu swali moja au mawili kutoka katika kila sehemu ya wazo uamuzi utafanywa ili kupata matokeo yanayohitajika.
Tafsiri
Katika jamii ya wingilugha, ni muhimu kwamba kila mlengwa anastahili kujibu maswali katika lugha anayoifahamu vyema.
Hata ingawa jambo hili huhitaji muda mwingi, njia mwafaka ya kuhakikisha kwamba maana ya hojaji hubakia asilia hata baada ya kutafsiriwa, ni kwa kutumia njia ya “upofu-kuwili” double blind. Kundi moja la wanaisimu lipewe hojaji asilia na kuitafsiri katika lugha lengwa. Kisha, kundi lingine la wanaisimu lipewe zile tafsri zilizo katika lugha lengwa na kuzitafsiri tena katika lugha ya Kiingereza (lugha yake asilia).
Kwa wakati huu, tafsiri zilizotafsiriwa tena kutoka lugha lengwa hadi lugha asilia zichunguzwe dhidi ya matini asilia. Tofauti zitakazojitokeza zinahitajika kupatanishwa kwa kutafuta neno jingine badalia kutoka kwa lugha asilia au lugha lengwa linalofidia maana asilia. Tanbihi; hata hivyo, iwapo matini asilia yatabadilika, tafsri nzima yastahili kuchunguzwa tena.
Watafsiri wema huwa hawatafsiri neno kwa neno. Huhitaji kuelewa lini walengwa wanaweza kutumika katika maneno muhimu wanayoyasikiza kwa lugha nyingine, kama vile “bunge” ndipo neno mwafaka litumike.
Njia ya Mahojiano
Mahojiano ni njia mwafaka ya utafiti. Majibu kwa maswali ya utafiti si lazima yawe huru kutokana na yalivyoulizwa.
Simu
Njia inayoendelea kupata umaarufu sana kuwahoji walengwa ni ya simu. Utafiti wa simu huwa wa haraka na si ghali kwa vile hauhitaji mtafiti kusafiri nchini au maeneo fulani na kwa maboma ya watu ili kukutana na wahojiwa.
Hata hivyo, changamoto kubwa ni idadi halisi ya wanaomiliki simu. Hata kule Marekani mnamo mwanzo wa miaka ya 1990 imekadiriwa kwamba asilimia tano ya idadi ya taifa na hata asilimia kumi katika baadhi ya majimbo hawakuwa na simu.
Tatizo kubwa ni kuwa umiliki wa simu si nasibu. Kwa kiwango kikubwa huhusishwa na kipato cha kaya. Wale ambao hawamiliki simu huenda wakawa na maoni tofauti kabisa ya kijamii na kisiasa ikilinganishwa na wale wanaomiliki simu. Katika mataifa yanayoendelea, kuwepo kwa wamiliki wachache wa simu na wasiolingana, hufanya utafiti wa kitaifa usiwezekane, kwani haufumbati kaya za wenye mapato ya chini.
Kule Marekani, shirika la Gallup kwa wakati mmoja lilikadiria kuwa utafiti wa kura za maoni kupitia kwa simu zilipendelea wagombezi wa WanaJamhuri kuliko wale wa WanaDemokrasia. Dhibitisho halisi kule Afrika Kusini lilitokea mnamo mwaka wa 1992 wakati shirika la Human Science Research Council(HSRC) lilitumia utafiti wa simu katika kura za maoni za wagombezi wa urais na kuonyesha kuwa F.W. de Klerk alikuwa na wanaomuunga mkono wengi kumliko mpinzani wake, Nelson Mandela. Shirika la HSRC lilidai kwamba limechunguza vyema matokeo ya kura za maoni kwa misingi ya tofauti za rangi za wapiga kura nchini. Walichosahau ni kwamba wale Waafrika waliomiliki simu hawangewakilisha Waafrika wote kwa ujumla.
Tafiti za simu pia huwafanya watu kujiondoa katika utafiti na hivyo kuondoka kwenye sampuli. Kama ilivyodokezwa pale chini ni muhimu kutowaruhusu watu kujiamuliaa wenyewe kujiondoa kwenye sampuli. Aidha, mahojiano ya simu huwa hayaleti maelewano kamili ya mahojiano ya masuala ya kibinafsi. Ni muhimu kwa mtafiti kuwaelekeza wahojiwa katika masuala ya kibinafsi yanayoleta utata.
Watu huwa hawako huru kuelezea mielekeo hasi kwa watu wasiofahamu au hata bila kuonana nao ana kwa ana. Kunayo mapendeleo kwa data ambayo si hasi kwani sampuli za simu pia huweza kuhusisha wageni. Hata hivyo, wakati mwingine ukosefu wa kuonana ana kwa ana kwa watafiti na walengwa hufanya tafiti za simu kupendelewa.
Posta/Barua
Katika utafiti kwa njia ya posta, hojaji hutumwa kwa walengwa kupitia kwa posta. Hojaji huwa yenye mtiririko. Njia hii huhusisha shughuli kiasi na gharama ya kutuma kwa njia ya posta hivyo njia hii si ghali mno.
Kwa upande mwingine njia ya posta huwa na matokeo yasiyoridhisha. Kupata thuluthi moja au robo moja ya majibu kutoka kwa wahojiwa huchukuliwa kama ushindi mkubwa. Hata hivyo, majibu ya aina hii huhitaji juhudi kubwa kuwakumbusha wahojiwa mara mbili au tatu ili kuwashawishi kujaza na kurudisha majibu yao. Wakati mwingine wahojiwa huhitaji kutiwa motisha kwa kuwapa tuzo au fursa ya kujinyakulia nafasi za kushinda tuzo wakijaza na kurudisha hojaji walizotumiwa.
Mahali pengine, matokeo yanayotakiwa ya tafiti za njia ya posta hulemazwa na viwango vya huduma za posta na viwango vya juu vya kutojua kusoma na kuandika. Kutokana na sababu hizi na nyinginezo, tafiti za posta hufanywa tu kwa wahojiwa maalumu kutokana na jumuiya, hasa zaidi walengwa walioelimika, mameneja wa viwango vya juu au waamuzi wa kielimu.
Mahojiano ya kibinafsi
Mahojiano ya kibinafsi hujengwa kati ya mtafiti na mhojiwa. Jambo hili huwezesha mtafiti kuuliza maswali tata zaidi na kupata majibu ya kina. Sifa za mtafiti kama vile rangi na uana huenda zikamwathiri mhojiwa kuelezea masuala ya kijamii yasiyotamanika hasa kuhusu rangi na uana. Hali hii hutokana na kuonana ana kwa ana kwa mtafiti na mhojiwa. Kwa hivyo, mahali kama Afrika Kusini, mashirika ya utafiti hujaribu kuhakikisha kwamba wahojiwa ni wa rangi moja na watafiti. Iwapo utafiti ulikuwa unahusu jinsia au masuala ya uana, juhudi zilifanywa kuwa watafiti watakuwa wa jinsia moja na wahojiwa wao.
Mahojiano ya kibinafsi hujitokeza kuwa ghali kutokana na kazi inayohusika na gharama za usafiri. Pia tafiti za mahojiano ya kibinafsi hukumbwa na pingamizi za utaratibu ambazo hazipatikani katika njia zingine za utafiti. Kwa mfano, kuna matazamio ya kupita mbele ya lango kuu la mtu sio tu kuingia ndani. Katika Afrika kusini kuna dhana ya ujirani “mbaya”, mfumo wa ulinzi na matatizo mengine madogo madogo kama vile Rotweiller au mbwa wa Doberman Pinscher ambao huzuia watafiti kuhoji kila mtu katika sampuli.
Vilevile, wale umbao watakataa kuhojiwa au wasiofikika kwa mahojiano waweza kutia dosari kwa sampuli kwani watu hawa huenda wakawa na fikra na mielekeo tofauti na jumuiya.